WANAFUNZI
14,000 kati ya 40,000 walioomba kujiunga na masomo ya juu wamechaguliwa
kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) katika mwaka mpya wa
masomo 2017/18 unaoanza wiki hii.
Mkurugenzi wa Shahada za Awali katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Profesa Allen Mushi alisema hayo juzi. Alisema kulikuwa na ushindani
mkubwa na waliochaguliwa ni waliopata alama za juu zaidi.
Alisema changamoto waliyokutana nayo katika udahili ni kuwa wanafunzi
wengi waliomba chuo zaidi ya kimoja, hivyo pale chuo kinapowakubalia
hakijui ni wangapi watakwenda hapo hivyo hilo liliwasumbua.
Alisema kutokana na hali hiyo, chuo kilitoa nafasi kwa wanafunzi
waliochaguliwa kuthibitisha kujiunga chuoni hapo. “Hali hii imetufanya
tufungue mtandao mara tatu ili watu ambao hawakupata waombe upya kujaza
nafasi za ambao hawakuthibitisha kujiunga na chuo baada ya kukubaliwa,”
alisema Profesa huyo.
Alisema awamu ya kwanza wanafunzi 2,800 hawakuthibitisha hivyo mtandao
ulifunguliwa na ya tatu pia ulifunguliwa ili kutoa haki kwa waliosema
mtandao uliwasumbua au walichelewa kupata taarifa hizo.
Alisema mfumo wa mwaka huu wa kutoa uhuru kwa mwanafunzi kuchagua chuo
anachokipenda ni mzuri lakini changamoto ni wanafunzi kuomba zaidi ya
chuo kimoja kuogopa kukosa kabisa walikotarajia.
Ofisa Mahusiano ya Umma UDSM, Jackson Isdory alisema wanafunzi wa mwaka
wa kwanza watafungua chuo Oktoba 28, mwaka huu na wanaoendelea Novemba
4. Alisema wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanawahi ili kupewa maelekezo na
taratibu za chuo hicho, kuyajua mazingira yake na pia kujisajili chuo.
SOURCE @Habarileo



No comments:
Post a Comment