Viongozi wa kisiasa wa Ujerumani wanakusanyika Jumanne katika mji wa
mashariki wa Wittenberg Ujerumani, ili kuadhimisha miaka 500 ya
mabadiliko yaliyoanzisha kanisa la Waprotestanti.
Ni katika mji huo ambapo kasisi wa Kijerumani Martin Luther aliongoza
mgawanyiko katika Kanisa Katoliki katika mojawapo ya matukio muhimu
zaidi barani Ulaya.
Akiwa profesa wa thiolojia na kasisi, Luther alipinga mamlaka ya Vatican
na alitilia shaka mafundisho ya Kanisa Katoliki na yaliyofanywa na
Kanisa hilo kupitia ile michanganuo yake maarufu 95. Anaaminika kuwa
aliibandika michanganuo hiyo katika mlango wa kanisa la Wittenberg mnamo
Oktoba 31 mwaka 1517.
Kama kumbukumbu nyengine zote za Luther katika jimbo la Saxony-Anhalt
mashariki mwa Ujerumani, mlango wa kanisa hilo umeorodheshwa kama
kumbukumbu muhimu na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na
utamaduni UNESCO.
Viongozi mashuhuru wanatarajiwa kuhudhuria
Rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier, Kansela Angela Merkel na Mkuu
wa jimbo la wa Saxony-Anhalt Reiner Haseloff pamoja na wageni wengine
wengi mashuhuri kutoka Ujerumani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria
sherehe hiyo.
Kansela Merkel amesema sherehe hii ambayo ni siku ya ya kitaifa
Ujerumani, inatoa nafasi ya kutafakari mageuzi yaliyotokana na
mabadiliko hayo yaliyoletwa na Martin Luther.
Wanamziki pamoja na wachekeshaji ni miongoni mwa watu wanaotarajiwa
kuwepo katika sherehe hizo katika harakati za kuzifufua fikra za enzi
ambazo Martin Luther alikuwa akiishi bado.
Zaidi ya hayo, kuna mpango wa maonesho ya sanaa pamoja na tamasha la
mataa na katika sehemu zengine za nchi, msururu wa mambo ya kuadhimisha
mabadiliko aliyoyaleta Luther yanaendelea.
Huku hayo yakiarifiwa zaidi ya watu 600 katika mji wa Kusini Magharibi
wa Mannheim, waliandika kwa mkono tafsiri ya Biblia, kama mojawapo ya
njia za kusherehekea maadhimisho ya miaka 500 ya mabadiliko.
Huko Mannheim watu wanafanya tafsiri ya Biblia kuadhimisha siku hii
Kasisi Stefan Scholpp kutoka kanisa la Kiinjili katika eneo hilo
anasema, "washiriki walikuwa kati ya umri wa miaka 8 hadi 99 na
wanawakilisha watu wengi wa matabaka mbali mbali," alisema Scholpp,
"kutoka kanisa la Kiinjili la Ujerumani, mwenyekiti wa baraza Heinrich
Bedform-Strohm, hadi mfungwa aliye katika gereza la Mannheim," aliongeza
Kasisi huyo.
Baada ya kufanya tafsiri, kulikuwa na wahariri waliokuwa wanapitia kile
kilichoandikwa na washirika katika mradi huo wa kuitafsiri Biblia, na
Scholpp amesema walilazimika kusahihisha makosa kadhaa ingawa hakuna
wakati wowote ambapo walikumbana na kisa ambapo kulikuwa na mtu
aliyekufuru katika kutafsiri.
Yatakayotokana na mradi huo ulioanza mwezi Aprili, yatajumuishwa katika
kitabu kikuu kitakachokuwa na kurasa 3,626 na Scholpp anapanga kuitumia
Biblia hiyo kama Biblia ya altare katika kanisa lake huko Mannheim.



No comments:
Post a Comment